Archive for July 4, 2017

Ujenzi Wa Sehemu Ya Kujifungua Kina Mama Hospitali Ya Mpeketoni

Gavana wa kaunti ya Lamu Issa Timamy mnamo tarehe 01/07/2017 ameweka jiwe la msingi ili kujenga sehemu ya kujifungua kinamama katika hospitali ndogo ya kaunti huko Mpeketoni.

Sehemu hiyo ya kujifungulia kina mama ya ghorofa, itakuwa na uwezo wa kupokea wazazi zaidi ya 30 na kugharimu takriban shilingi milioni 50 za Kenya.

Jengo hilo la kisasa pia litakuwa na chumba chake cha upasuwaji na pia sehemu ya kina mama kujifungua kwa njia ya kawaida.

Aidha gavana Timamy alikabidhi sehemu ya ardhi katika hospitali hiyo ya Mpeketoni kwa mwanakandarasi ili  kujingwa sehemu ya kufulia nguo za hospitali kabla ya kupanda mti kwenye ardhi ya hospitali hiyo.

Pia alitembelea shule ya upili ya wavulana ya Mpeketoni kukagua ujenzi unaoendelea wa maktaba ya kisasa shuleni humo.

Upimaji Wa Mji Wa Witu

Gavana wa Lamu Issa Timamy hapo jana 03072017 alizindua rasmi upimaji na upangaji wa mji wa Witu katika eneo la Kamkunji.

Shughuli hii inatarajiwa kukamilika kwa mda wa mwezi mmoja huku wakaazi 2500 wakitazamiwa kunufaika na upimaji huu.

Zoezi hili litajumuisha nyumba za zamani za mji wa Witu na zile za mji mpya.

Gavana Timamy ameitaka kamati iliyochaguliwa kusimamia zoezi hilo kuhakikisha kuwa usawa na haki umetendeka bila ya ubaguzi.

Aidha amewaonya wale walionyakua ardhi kuwa ardhi hizo zitagawiwa wenyeji na kusema kuwa si haki kwa mtu mmoja kuchukua sehemu kubwa ya ardhi huku wengine wakiwa hawana hata kipande.

Wakati huo huo gavana Timamy alitembelea eneo la Kitumbini na kuahidi kukarabati eneo la kuogeshea ngombe ambalo limeachwa kwa miaka mingi.