Gavana Wa Lamu Akutana Na Wahundumu Wa Afya Katika Hospitali Ya King Fahad

Gavana wa Lamu Fahim Twaha amekutana na wahudumu wa afya katika hospitali ya King Fahad na kutaka kusikia kilio chao kufuatia mgomo wa wauguzi na maafisa wa kiliniki unaoendelea.

Wakitoa malalamishi yao wafanyikazi hao wa afya wamemuelezea gavana Twaha kuwa hawakuridhishwa na mabadiliko yaliyofanywa na tume ya kukadiria mishahara ya wafanyikazi wa umma (SRC)ambapo wameteremshwa daraja.

Aidha wamemuelezea gavana Twaha kuwa tume hiyo ya kukadiria mishahara imewapatia mambo ambayo hawakuitisha.

Wafanyikazi hao wa afya wamemtaka gavana Twaha kuchukua malalamishi yao na kuyawasilisha kwa baraza la magavana nchini  ili yazingatiwe.

Kwa upande wake gavana Twaha amewahakikishia wafanyikazi hao kuwa atafanya kila liwizalo kuhakikisha kuwa matakwa yao yamezingatiwa.

Aidha gavana Twaha ametoa wito kwa  wafanyikazi hao wa afya kutumia njia ya mazungumzo kwanza kabla ya kuchukua hatua za kugoma.

Twaha amesema mlango wake uko wazi na wakati wowote wanapomuhitaji yuko tayari kuwasikiliza.

Baada ya kikao hicho na wafanyikazi wa sekta ya afya katika hospitali ya King Fahad gavana Twaha alifululiza hadi katika hospitali ya Mpeketoni ili kukutana na wafanyikazi wake.

Aidha hapo kesho atatembelea hospitali ndogo ya kaunti huko Faza.

 

Trackback from your site.

Leave a comment

*