Naibu Gavana,Dkt. Mbarak afanya Mazungumzo na Walimu na Kukaguwa Mradi wa Maji Shuleni.
Naibu Gavana wa Kaunti ya Lamu, Dkt. Mbarak M. Bahjaj, hapo Jana ametembelea Shule ya Wadhajir Kilimani pamoja na Safirisi katika eneo bunge la Lamu Magharibi, ambako alifanya mazungumzo na walimu na kukagua maendeleo ya mradi wa kisima unaoendelea shuleni humo.
Mradi huo wa kisima unafadhiliwa na shirika la Helping Hand Charitable Organization kwa ushirikiano na afisi ya Naibu Gavana Daktari. Bahajaj, na unatarajiwa kukamilika ndani ya wiki moja ijayo.
Kazi zinazotekelezwa ni pamoja na uwekaji wa tanki la kuhifadhia maji na usambazaji kupitia mabomba matatu yatakayosaidia upatikanaji wa maji safi kwa urahisi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Bahjaj alisisitiza dhamira na malengo ya utawala wa Gavana Issa Timamy katika kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi kote Kaunti ya Lamu.
Alieleza kuwa upatikanaji wa maji safi utasaidia kumaliza changamoto ya uhaba wa maji mashuleni, kuimarisha programu za lishe shuleni, pamoja na kuboresha viwango vya usafi kwa wanafunzi na walimu.
Aidha, Naibu Gavana alibainisha kuwa ofisi yake itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha shule zinapata vifaa vya kujifunzia pamoja na huduma muhimu kama maji safi, kwa lengo la kuinua ubora wa elimu katika kaunti hiyo.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za serikali ya kaunti kuhakikisha kila mwanafunzi anapata mazingira salama na bora ya kujifunzia.
– Mwisho –
Kwa maelezo zaidi, wasiliana na:
Ofisi ya Mawasiliano
Barua pepe: communication@lamu.go.ke



