ATC Mpeketoni, yafufuliwa Upya

Mstahiki gavana Issa Timamy mapema leo amefungua rasmi siku tatu za Maonyesho na mafunzo ya Kilimo cha kisasa katika eneo la ATC Mpeketoni.

Akiandamana na Naibu wake Raphael Munywa Gavana Timamy, alitembelea vibanda vya mashirika na kampuni zinazouza mbegu na mbolea.

Kauli mbiyu ya Maonyesho haya ni:-

“kutumia teknolojia ya kilimo endelevu kwa usalama wa chakula na kuongeza kipato”

Kwenye Maonyesho hayo wakulima watapata fursa ya kujifunza mbinu mbali mbali za Kilimo pamoja na njia bora za kutumia dawa za kuzuwia wadudu kwa mimea.

Akihutubia wakulima na wananchi waliohudhuria Maonyesho hayo gavana Timamy, amewaomba wakulima kutosheka na mbegu walizopata huku akiahidi kuongeza fedha katika mgao wa bajeti ya mwaka ujao wa kifedha ili kuagiza mbegu za kutosha.

“Serikali yangu imekuta bajeti finyu nami nimeongeza ndio hii mbegu imepatikana kwa hivyo nawasihi tusiingize siasa swala hili” Timamy alisema.

Aidha, amesema watawalekeza wakulima kununua mbegu na dawa ambazo zitajaribiwa na kufaulu hapo ATC.

Kufunguliwa tena kwa ATC kwa wakulima kumerejesha matumaini kwa wakaazi wa kaunti ya Lamu dhidi ya Kilimo.

Wakati huo huo Gavana ametangaza kuwa mwezi wa nane serekali yake itaandaa Maonyesho ya Kilimo Mpeketoni ambayo huenda yakafunguliwa rasmi na Waziri wa Kilimo nchini.

Waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na:- Mkuu wa wafanyikazi Abdulnasir M Issa,Waziri wa Kilimo James Gichu, Waziri wa Elimu Sabastian Owanga, Waziri wa Fedha Mohamed Bwana , Mwakilishi wa wadi ya Bahari Francis Gakonga miongoni mwa wengine.