*KAUNTI YA LAMU YAZINDUA HUDUMA ZA AFYA MASHINANI [TimamyCare]*

Gavana wa Lamu Mstahiki Issa Timamy E.G.H, O.G.W asubuhi ya leo, amezindua upya huduma ya afya mashinani katika makao makuu ya afisi za kaunti ya Lamu, Mokowe.

Huduma hiyo ya gari ambayo itawafikia wenyeji vijijini mwao, itafahamika kama *Timamy Care* Afya Mashinani, Afya Majumbani .

Huduma hizi zitatolewa na wahudumu wa afya wa kaunti wakishirikiana na wale wa kujitolea katika sehemu za ndani.

Akizungumza wakati wa kuzindua gari ambalo litatumika kutoa huduma hiyo, Gavana Issa Timamy, amewapongeza wahudumu wa afya wa kujitolea kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya ya kushugulikia wagonjwa mashinani.

“Kama hakikisho la kudumisha uhusiano mwema baina ya serikali na wahudumu wa afya wa kujitolea, serikali yangu itapendekeza kujumishwa kwa wahudumu wa kujitolea kwenye bajeti ya mwaka wa 2023/2024 ili wapate kiinua mgongo kutokana na kazi yao nzuri” Asema Gavana.

Kwa upande wake,Naibu Gavana Raphael Munywa,aliwapogeza wahudumu hao kwa kujitolea kwao na kuwaomba waendelee na juhudi zao za kutoa huduma afya kwa ushirikiano na idara ya afya.

Waziri wa Afya Daktari. Mbarak Mohamed Bahajaj, alimshukuru Gavana Timamy kwa kujitolea kuboresha huduma za afya huku akitoa hakikisho kuwa idara yake imeweka mipango mahususi ili kuboresha huduma za afya.

Gari hilo ambalo ni la kipekee, lilikarabatiwa na kuweka vifaa vya kutoa matibabu ya afya, limerejelea kutoa huduma baada ya kutelekezwa miaka mitatu iliyopita litakuwa likitembea vijijini kutoa huduma za afya mara moja kwa wiki.

Waliokuwepo ni pamoja na Mkuu wa Utumishi wa Umma Balozi Ali Abbas, Msimamizi wa afisi ya Gavana Abdulnasir M. Issa, Afisa Mkuu wa Uhasibu Dkt. Victor Tole miongoni mwa wengine.

-Mwisho-

Kwa habari zaidi tufikie kupitia;

communication@lamu.go.ke