Serekali ya kitaifa itaharakisha mchakato wa kupatikana kwa kibali cha Baraza la Usimamizi Baharini (Marine Stewardship Council – MSC Certification) kwa wavuvi wa Kamba mawe kaunti ya Lamu.

Akiwa na mazungumzo ya kina na Gavana Issa Timamy afisini mwake mapema hii leo,Waziri wa Madini, Uchumi Samawati na Shughuli za Baharini Salim Mvuriya, amesema hatua hii itatoa nafasi ya kufikia soko la Umoja wa Ulaya ambapo Kamba hao watasafirishwa.

Aidha Waziri Mvuriya amesema, kwa usaidizi kutoka kwa serekali ya kitaifa, kaunti ya Lamu itaanzisha Chuo cha mafunzo ya Baharini kwenye kituo cha kutoa maelekezo Baharini kichoko kwa sasa.

Pia wavuvi wa ndani watafanyiwa mafunzo ya ubaharia na kupewa cheti bila ya kupitia mafunzo maalum na kutengwa fedha ili kujenga kiwanda cha Kusindika Samaki Lamu.

Nao mradi wa KEMFSED utawekeza kwa boti za wastani za uvuvi wa bahari kuu ili kuwezesha kutumia rasilimali nyingi zilizoko katika bahari ya Lamu.

Wakati huo huo, waziri Mvuriya akiwa na mwenyeji wake Gavana Issa Timamy na wakuu wengine serekalini walizuru afisi ya Kamishna wa Kaunti ya Lamu Irungu Macharia kabla ya kutembelea bandari ya Lamu.

-Mwisho-