Gavana Issa Timamy azindua rasmi utowaji wa mbegu kwa wakulima katika wadi ya Faza

Serekali ya Kaunti ya Lamu kupitia Idara ya Kilimo hii leo imeanzisha rasmi zoezi la kupeana mbegu kwa wakulima wote walioko katika wadi ya Faza kwa ajili ya upanzi mbele ya msimu wa mvua inayotarajiwa kunyesha.

Wakulima 1300 kutoka barani na visiwani wadi ya Faza wamelengwa kupokea tani 14 za mbegu zikiwemo zile za mahindi, pojo, kunde, mchele na mtama.

Akizundua rasmi zoezi hilo huko Faza, Gavana Issa Timamy akiwa ameandamana na Naibu wake Raphael Munywa, amewaahidi wakulima kuwa baada ya wiki mbili hivi boti iliyokuwa ikisafirisha wakulima na mazao yao hadi barani itaregelea shughuli zake.

“Hii boti malengo yake ilikuwa ni kusafirisha wakulima hadi barani lakini imeharibiwa na inakarabatiwa na baada ya wiki mbili au tatu itakuwa tayari na nimeagiza irudishwe huku” Gavana alihakikishia wakulima.

Aidha, Timamy ametoa wito kwa kulima kupanda mbegu na kutojaribu kuzitumia kama chakula.

Shughuli hiyo ya utowaji wa mbegu kwa wakulima itaendela katika wadi zote za Kaunti ya Lamu.

Waliohudhuria ni pamoja na katibu mkuu wa kaunti Balozi Ali Abbas, Afisa mkuu wa wafanyikazi Abdulnasir M Issa, waziri wa Kilimo James Gichu, Mwakilishi wa wadi ya Faza Mohamed Aboud miongoni mwa wengine.

-Mwisho-

Kwa habari zaidi wasiliana nasi kupitia afisi ya mawasiliano kutumia; communication@lamu.go.ke